MTU AKIFA, KUNA NINI BAADAYE?

Tunajikunyata mtoto mdogo anapouliza kwanza swali hili, "kufa maana yake nini? Tunaywea kuzungumza au hata kufikiri juu ya mtu fulani tumpendaye anapokaribia kufa. Mauti ni adui wa watu wote kila mahali.

Je! majibu ni yapi kwa maswali magumu yahusuyo kifo? Je! kuna maisha baada ya kufa? Je! tutawaona tena wapendwa wetu waliokufa?

1. Kukikabili Kifo Bila Hofu

Sisi sote kwa wakati fulani, labda baada ya kufa rafiki yetu au mpendwa wetu, tumejisikia kana kwamba tumbo liko tupu, yaani, kuwa na hisia ile ya upweke inayopita ndani yetu tunapoangalia kwa haraka kuona mwisho wa uhai wa mtu.

Katika jambo hili la maana sana, lililojaa hisia nyingi, ni wapi basi, tunakoweza kujifunza habari za kile kinachotokea tunapokufa? Kwa bahati nzuri, sehemu ya utume wa Kristo hapa duniani ilikuwa ni "kuwaweka huru wale ambao katika maisha yao yote walikuwa katika hali ya utumwa kwa hofu ya mauti" (Waebrania 2:15). Na katika Biblia, Yesu anatoa ujumbe wenye faraja, kisha anajibu maswali yetu yote juu ya mauti na yale maisha ya baadaye kwa njia inayoeleweka wazi.

2. Jinsi Mungu Alivyotuumba

Kuelewa kutoka katika Biblia ukweli halisi juu ya kifo, hebu na tuanze mwanzo na kuona jinsi Mungu alivyotuumba.

"BWANA Mungu akamfanya mtu (Adamu, Kiebrania) kwa MAVUMBI YA ARDHI (adamah, Kiebrania), akampulizia puani PUMZI YA UHAI, na mtu yule akawa NAFSI HAI [roho, Kiebrania]." - (Mwanzo 2:7).

Wakati ule wa uumbaji, Mungu alimfinyanga Adamu kutoka katika "mavumbi ya ardhi." Alikuwa na ubongo kichwani mwake ulio tayari kufikiri; damu katika mishipa yake iliyo tayari kuzunguka mwilini mwake. Ndipo Mungu alipompulizia puani "pumzi ya uhai," na Adamu akawa "nafsi hai" [Kiebrania, "roho hai"]. Zingatia kwa makini, Biblia haisemi Adamu alipokea roho; bali inasema tu kwamba "mtu akawa roho hai." Mungu alipompulizia Adamu pumzi puani mwake, uhai ukaanza kuingia ndani yake kutoka kwa Mungu. Mwungano huo wa mwili na "pumzi ya uhai" ulimfanya Adamu kuwa "nafsi hai," tunaweza kundika mlinganyo (equation) wa kibinadamu kama hivi:

"Mavumbi ya Ardhi" + "Pumzi ya Uhai" = " Roho Hai"

Mwili Usio na Uhai + Pumzi toka kwa Mungu = Nafsi Hai.

Kila mmoja wetu anao mwili na akili inayofikiri. Kwa kadiri sisi tunavyoendelea kuvuta pumzi, tutaendelea kuwa nafsi hai, yaani, roho hai.

3. Kunatokea Nini Mtu Akifa?

Mtu anapokufa kinyume cha hatua zile za uumbaji zilizoelezwa katika Mwanzo 2:7 hutokea "Nayo MAVUMBI huirudia ardhi yalikotoka, nayo ROHO [PUMZI YA UHAI] humrudia Mungu aliyeitoa." - (Mhubiri 12:7).

Mara nyingi Biblia hutumia maneno ya Kiebrania yamaanishayo "pumzi" (breath) na "roho" (spirit) kwa kubadilishana. Watu wanapokufa, mwili wao unageuka na kuwa "mavumbi" na "roho ("pumzi ya uhai") humrudia Mungu aliyeitoa. Lakini, je! kunatokea nini kwa ile roho hai (living soul)?
"Kama mimi niishivyo, atangaza Bwana Mungu,…. Kila ROHO ILIYO HAI (LIVING SOUL) ni mali yangu;… ROHO YULE ATENDAYE DHAMBI NDIYE ATAKAYEKUFA." - Ezekieli 18:3-4.

Roho inakufa! Kwa sasa haina uwezo wa kuishi milele - inaweza kuangamizwa. Mlinganyo ule ulioupata kutokana na Mwanzo 2:7, Mungu alipotuumba sisi, unajipindua wakati ule wa kufa.
"Mavumbi ya Ardhi" - "Pumzi ya Uhai" = "Roho Iliyokufa"
"Mwili usio na uhai - Pumzi toka kwa Mungu = Nafsi Iliyokufa.

Mauti ni kukoma kabisa kwa uhai. Mwili unavunjika-vunjika na kugeuka kuwa mavumbi, na ile pumzi, au roho, humrudia Mungu. Sisi ni roho hai tunapoendelea kuishi, lakini tunapokufa tunakuwa maiti tu, yaani, roho iliyokufa, nafsi iliyokufa. Kwa hiyo wafu hawana fahamu zo zote. Mungu anapoiondoa kwetu pumzi yake ya uhai aliyotupa, roho yetu hufa. Lakini kama tutakavyoona baadaye katika somo hili, tukiwa na Kristo tumaini liko.

4. Mfu, Anajua Kiasi Gani?

Baada ya kufa ubongo unaharibika; hauwezi kujua, wala kukumbuka kitu cho chote. Hisia zote za moyo za kibinadamu hukoma kabisa mtu anapokufa.

"Upendo wao, chuki yao na wivu wao, vimetoweka siku nyingi sana…" - (Mhubiri 9:6).

Wafu hawana fahamu zo zote, hivyo hawana habari na kitu cho chote kinachotokea hapa. Hawana mawasiliano yo yote na wale walio hai:
"Kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa, lakini WAFU HAWAJUI CHO CHOTE." - (Mhubiri 9:5).

Kifo ni kama usingizi usio na ndoto - kwa kweli, Biblia inakiita kifo kuwa ni "usingizi" mara 54. Yesu alifundisha kwamba kifo ni kama usingizi., alisema hivi kwa wanafunzi wake:
Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha". Wanafunzi wake wakamwaabia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona". Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. Basi, Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa;- (Yohana 11:11-14).

Lazaro alikuwa amekufa yapata siku nne kabla Yesu hajafika pale. Lakini Yesu alipokwenda kwenye kaburi lake, alithibitisha kwamba kwa Mungu ni rahisi kuwafufua wafu kama ilivyo rahisi kwetu kumwamsha mwenzetu aliyelala usingizi.

Ni faraja kubwa kwetu kujua kwamba wapendwa wetu waliokufa wame "lala usingizi," yaani, wanapumzika salama salimini ndani ya Yesu. Shimo lile refu la mauti, ambalo sisi wenyewe tutalipitia siku moja, ni kama kulala usingizi mtulivu wa amani.

5. Je! Mungu Anawasahau Wanaolala Usingizi Wa Mauti?

Usingizi huo wa mauti sio mwisho wa kisa hiki. Pale kaburini, Yesu alimwambia Martha, dada yake Lazaro, maneno haya: "MIMI NDIMI HUO UFUFUO, na uzima. YEYE ANIAMINIYE MIMI ATAKUWA ANAISHI, HATA KAMA ATAKUFA." - (Yohana 11:25).

Wale wanaokufa "katika Kristo" wanalala usingizi makaburini mwao lakini wao bado wanalo tumaini zuri la kupata maisha yale ya baadaye. Yeye anayeuhesabu kila unywele juu ya vichwa vyetu na kutushika katika kiganja cha mkono wake hatatusahau sisi. Tunaweza kufa na kurudi mavumbini, lakini kumbukumbu ya utu wetu bado i wazi katika mawazo ya Mungu. Na Yesu atakapokuja, atawaamsha wenye haki waliokufa kutoka katika usingizi wao, kama vile alivyofanya kwa Lazaro.

"Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. Basi, farijianeni kwa maneno haya" - (1 Wathesalonike 4:13, 16-18).

Siku ile ya ufufuo lile shimo refu la mauti litaonekana kana kwamba ni pumziko letu la muda mfupi sana. Wafu hawana habari na muda unaopita. Wale waliompokea Kristo kama Mwokozi wao, wataamshwa kutoka usingizini kwa sauti yake ya ajabu ikishuka kuja hapa duniani.

Tumaini hilo la ufufuo linaye mwenzake; yaani, tumaini la kuwa na makao yale ya mbinguni ambako Mungu "atafuta kila chozi katika macho yao." Mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu" (Ufunuo 21:4). Wale wanaompenda Mungu hawana haja ya kuogopa mauti. Ng'ambo yake kuna umilele wa maisha yale matimilifu pamoja na Mungu. Yesu anazo "funguo za mauti" (Ufunuo 1:18). Bila Kristo, mauti ingekuwa ni njia ya moja kwa moja inayoishia katika hali ya usahaulifu kabisa, lakini tukiwa pamoja na Kristo, basi, kuna tumaini linalong'aa, lenye furaha.

6. Je! Tuna Miili Isiyokufa Sasa?

Mungu alipomwumba Adamu na Hawa, waliumbwa wakiwa na miili inayokufa, yaani, walikabiliwa na kifo. Laiti kama wangaliendelea kuwa watii kwa mapenzi yake Mungu, wasingeweza kufa kamwe. Lakini
walipotenda dhambi, walipoteza haki yao ya uzima. Kwa uasi wao ule wakakabiliwa na mauti. Dhambi yao iliwaambukiza wanadamu wote, na kwa kuwa wote wamefanya dhambi, basi, sisi sote tuna miili inayokufa, yaani, tunakabiliwa na mauti (Warumi 5:12). Wala hakuna dokezo hata moja katika Biblia lisemalo kwamba roho ya mwanadamu inaweza kuishi peke yake kama kitu kilicho na fahamu.

Kamwe Biblia haijaeleza hata mara moja kwamba roho kama ilivyo sasa ina hali hiyo ya kutokufa kamwe - yaani, kwamba haiwezi kufa. Maneno ya Kiebrania na Kigiriki ya neno hili "roho" (soul), na "roho" (spirit), na "pumzi" (breath) hutokea mara 1,700 katika Biblia. Lakini hakuna hata mara moja ambapo roho ya binadamu (soul), roho (spirit), au pumzi (breath) inatajwa kuwa haiwezi kufa. Kwa wakati huu wa sasa ni Mungu peke yake ambaye ana hali hiyo ya kutokufa kamwe.

"Mungu…. PEKE YAKE HAPATIKANI NA MAUTI." - I Timotheo 6:15,16.

Maandiko yanaeleza wazi kwamba katika maisha haya wanadamu wana hali ya kufa: yaani, wanakabiliwa na kifo. Lakini Yesu ajapo, mwili wetu utafanyiwa mabadiliko makubwa.

"Sikilizeni, nawaambieni siri sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa, wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutokuweza kufa tena, na sisi tutageuzwa. Maana ni lazima kila kuharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa"- (1Wakorintho 15:51-53).

Sisi, kama wanadamu, hatuna miili isiyokufa sasa. Lakini ahadi inayotolewa kwa Mkristo ni kwamba sisi tutakuwa na miili isiyoweza kufa kamwe wakati Yesu atakapokuja tena kwa mara yake ya pili. Uhakika wa ahadi ya uzima wa milele ulionyeshwa wazi Yesu alipolipasua kaburi lake na:
"Lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo" - 2Timotheo 1:10.

Mtazamo wa Mungu kuhusu mwisho wa wanadamu uko wazi: yaani, mauti ya milele kwa wale wanaomkataa Kristo na kuzing'ang'ania dhambi zao, au hali ya kutokufa kamwe kama zawadi kwa wale waliompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wao wakati ule atakapokuja.

7. Kukikabili Kifo Cha Mpendwa Wetu

Hofu zile ambazo kwa kawaida sisi tunapambana nazo tunapokabiliana na kifo zinakuwa kali sana wakati ule anapokufa mpendwa wetu. Upweke pamoja na ile hisia ya kupotelewa, mambo hayo yanaweza kutulemea sana. Suluhisho pekee kwa utungu huo uliosababishwa na kutengana na mpendwa wetu ni ile faraja tu atupayo Kristo. Kumbuka kwamba huyo mpendwa wako amelala usingizi, na wapendwa wako wanaopumzika katika Kristo watafufuliwa katika ule "ufufuo wa uzima Yesu atakapokuja."

Mungu anapanga maajabu yake ya kuwaunganisha tena wale waliotengana. Watoto wadogo watarejeshwa kwa wazazi wao waliojaa furaha kubwa. Waume na wake zao watakumbatiana. Utengano wa kikatili uliotokea katika maisha haya utakwisha. "Mauti imemezwa kwa ushindi"- (1 Wakorintho 15:54).

Wengine wanajisikia vibaya sana kutengwa na mpendwa wao kiasi kwamba wanajaribu kufanya mawasiliano na wapendwa wao waliokufa kupitia kwa mjumbe wa mizimu (spiritualist medium) au kwa mtu yule anayeunganisha mawasiliano kama hayo wa Kizazi Kipya (New Age Channeler). Lakini Biblia kwa njia ya pekee inatuonya sisi dhidi ya kujaribu kupunguza maumivu yetu yanayotokana na kufiwa kwa njia hiyo:
"Baadhi watawaambieni "Nendeni mkatake shauri kwa mizimu na mizuka iliayo kama ndege; kwani ni kawaida watu kutaka shauri kwa miungu yao; na kutaka shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai" - (Isaya 8:19).

Ndiyo, Hivi kwa nini? Biblia inaeleza waziwazi kwamba wafu hawana fahamu yo yote. Suluhisho la kweli kwa huo uchungu uliosababishwa na kutengwa na mpendwa wetu ni ile faraja ambayo ni Kristo tu awezaye kutupa. Kutumia muda wetu kuwasiliana na Kristo ni njia bora kabisa kiafya ya kukua kupitia katika hatua hizo za kuhuzunisha.

Kumbuka siku zote kwamba, kule kuzipata fahamu tena kwa wale walalao katika Kristo kutawajia wakati ule zitakapopigwa kelele za kuja mara ya pili kwa Kristo ambazo zitawaamsha wafu!

8. Kukikabili Kifo Bila Hofu

Kifo kinatunyang'anya sisi karibu kila kitu. Lakini kitu kimoja ambacho hakiwezi kutuondolea ni Kristo, na Kristo anaweza kukirudisha kila kitu mahali pake tena. Mauti haitatawala daima katika dunia hii. Ibilisi, waovu, mauti na kaburi vitaangamizwa kabisa katika lile "ziwa la moto" ambalo ni "mauti ya pili" (Ufunuo 20:14).

1. Hapa yapo mapendekezo manne rahisi juu ya kukikabili hicho kifo bila hofu: Uishi maisha ya kuwa na matumaini kwa kumtegemea Kristo, ndipo utakuwa tayari kufa dakika yo yote.

2. Kwa uweza wa Roho Mtakatifu, uwe mtiifu kwa amri zake Kristo, nawe utakuwa umejiandaa kwa yale maisha ya pili, ambayo ukiwa nayo hutaweza kufa kamwe.

3. Ifikirie mauti kama usingizi wa muda mfupi ambao kutoka katika huo sauti ya Yesu itakuamsha atakapokuja mara ya pili.

4. Itunze ile ahadi atupayo Yesu ya kutupa sisi makao yetu kule mbinguni kuishi pamoja naye milele hata milele.
Kweli ya Biblia humweka mtu huru mbali na ile hofu ya mauti kwa sababu inamfunua Yesu, ambaye hata mauti haikuweza kumshinda. Yesu anapoingia katika maisha yetu, anaigharikisha mioyo yetu na amani:
"Amani nawaachieni; amani yangu nawapa… Msifadhaike mioyoni mwenu , wala msiwe na woga." - (Yohana 14:27).

Yesu pia anafanya uwezekano uwepo kwetu wa kukabiliana na msiba unaotokana na kumpoteza mpendwa wetu. Yesu alitembea katika lile "bonde la uvuli wa mauti;" anaujua usiku mnene tunaoupitia.

"Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize Ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo" - (Waebrania 2:14,15).

Dk. James Simpson, tabibu mkuu aliyetengeneza ile dawa ya nusu kaputi [ya usingizi wakati wa upasuaji], alipatikana na hasara ya kutisha mtoto wake mkubwa kuliko wote alipokufa. Alihuzunika vibaya sana kama mzazi mwingine ye yote awezavyo kufanya. Lakini baadaye akaiona njia iliyomletea matumaini. Juu ya kaburi la mtoto wake yule mpendwa aliweka jiwe la kuonyesha alama na juu yake aliandika kwa kukata maneno haya ambayo Yesu alisema kuhusu ufufuo wake: "Na tazama, mimi ni hai."

Hayo ndiyo yote. Msiba wa mtu mmoja wakati mwingine unaweza kuonekana kana kwamba unaifutilia mbali ile mbingu; hata hivyo, Yesu yu hai! Mioyo yetu huenda ikawa ina huzuni nyingi sana; hata hivyo, Yesu yu hai!

Ndani ya Kristo tunalo tumaini la kuishi baada ya kifo chetu. Yeye ndiye "huo ufufuo, na uzima" (Yohana 11:25), naye anatoa ahadi hii kwetu, "kwa kuwa mimi ni hai ninyi pia mtakuwa hai" (Yohana 14:19). Kristo ndiye tumaini letu la pekee la kuwa hai kwetu baada ya kifo chetu. Na Kristo atakapokuja tena atatupa sisi uzima wa milele. Kamwe hatutaishi tena chini ya uvuli wa mauti, maana tunao uzima wa milele. Je! wewe umeligundua tumaini hili kuu ambalo tunaweza kulihifadhi moyoni mwetu katika zile nyakati zetu za giza nene kabisa? Kama wewe hujapata kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wako, je! utafanya hivyo sasa?

 

© 2004 The Voice of Prophecy Radio Broadcast
Los Angeles, California, U.S.A.