TOKA MDHAMBI MWENYE HATIA HADI MTAKATIFU ALIYESAMEHEWA

Hapakuwa na alama zo zote za vidole. Hakuna silaha yo yote iliyogunduliwa. Hakuna mtu ye yote aliyemwona mwuaji yule alipoingia katika ofisi ya yule daktari. Hakuna ye yote aliyesikia hata zilipofyatuliwa zile risasi. Lakini yule daktari alikuwa na risasi tano zimepenya shati yake.

Ilionekana kana kwamba ni uhalifu uliofanywa kwa ustadi sana. Mwanzoni Polisi hawakuweza kupata vidokezo vyo vyote. Lakini halafu waliona waya mwembamba sana uliofungwa kwenye chombo cha kuwekea kalamu ya risasi juu ya meza ya daktari yule. Waya ule ulikwenda kwenye kinasa sauti (tepurekoda) kilichokuwa ndani ya mtoto wa meza. Chombo kile cha kuwekea kalamu ya risasi, wakang'amua, kilificha hasa ile maikrofoni aliyoitumia yule daktari kuweka kumbukumbu ya mazungumzo yake na wagonjwa aliokuwa akiwapa ushauri.

Wapelelezi waliirudisha nyuma ile tepu ya kurekodia sauti, na kwa mshangao wao, wakaanza kuisikiliza ile tepu ilipofunguliwa tena kuhusiana na uhalifu ule wenyewe. Mtu aliyeitwa Antoni alikuwa ameingia katika ofisi ile na kuanza mabishano makali na yule daktari. Risasi zikafyatuliwa. Tepu ile iliishia na sauti ya maumivu makali ya daktari yule, aliyekuwa akifa juu ya lile zulia.

Kila habari ndogo ndogo ya kuogofya ilikuwa imerekodiwa. Yule mwuaji alidhani kwamba uhalifu wake ule ungebaki kuwa siri milele. Alikuwa mwangalifu sana kutokuacha kidokezo cho chote. Lakini ile tepu ilisimulia kisa chote.

Katika mwongozo huu tutajifunza habari za hukumu ya mwisho ya Mungu wakati wanadamu wanaendelea "kuhukumiwa sawa sawa na matendo yao kama yalivyorekodiwa katika vitabu vile" (Ufunuo 20:12). Kwa wale ambao hawajampokea Kristo kama Mwokozi wao, itakuwa ni habari mbaya kwao. Lakini hukumu hiyo ni habari njema za ajabu kwa wale walioupata usalama wao ndani yake Kristo.

1. Unaweza Kuikabili Hukumu Hiyo Bila Kuogopa

"Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote." - Yohana 5:22.

Ni kwa jinsi gani ule msalaba ulimwandaa Kristo kuwa Hakimu wetu?
"Mungu alimtoa [Yesu] kuwa kafara ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivyo ili kuonyesha wazi haki yake,… ili apate kuwa MWENYE HAKI NA MWENYE KUWAHESABIA HAKI wale wamwaminio Yesu" - (Warumi 3:25,26).

Kifo cha Kristo kama badala yetu kinamwezesha kufanya kazi yake kama Jaji mwenye haki, na Mwenye kuhesabia Haki aliye na rehema awezaye kumsamehe mwenye dhambi yule atubuye. Malimwengu yale yanayochungulia yanapouliza swali hili, "Je! yawezekanaje kwa Jaji yule asiyependelea kumtangaza mtu mwenye hatia kuwa hana hatia?" Kristo anaweza kutoa jibu lake kwa kuonyesha makovu katika viganja vyake. Amepata adhabu ya haki kwa ajili ya dhambi zetu katika mwili wake mwenywe.

Vitabu vile vya mbinguni hutunza kumbukumbu za maisha ya kila mtu mmoja mmoja, na kumbukumbu hizo zinatumika katika hukumu hiyo (Ufunuo 20:12). Hizo ndizo habari mbaya kwa wale wanofikiri kwamba dhambi zao za siri pamoja na uhalifu wao wanaoutenda havitarudi tena kamwe kuwasumbua. Lakini kuna habari njema za ajabu kwa wale wote waliompokea Kristo kwa moyo mnyofu kama mtetezi wao kule mbinguni. "Damu yake Yesu…. Yatusafisha dhambi yote" (1 Yohana 1:7).

Je, Yesu anatupa nini ili kubadilishana na maisha yetu ya dhambi?
"Mungu alimfanya [Kristo] aliyekuwa hana dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu ili ndani yake sisi tupate kuwa haki ya Mungu."- 2 Wakorintho 5:21.

Maisha yetu haya ya dhambi yanabadilishana na maisha yale makamilifu ya haki aliyokuwa nayo Kristo. Kwa ajili ya maisha yale yasiyo na dhambi na kifo chake Yesu, Mungu anaweza kutusamehe sisi na kututendea kana kwamba tulikuwa hatujapata kutenda dhambi kamwe.

Je, ni sifa gani alizo nazo Yesu ambazo zinamfanya kuwa Mtetezi na Jaji wetu?

2. Kristo Alikuja Wakati Ulipotimia

Wakati ule wa ubatizo wake, Yesu alipakwa mafuta na Roho Mtakatifu;
"Mara tu alipokwisha kubatizwa Yesu, alipanda kutoka ndani ya maji; dakika ile ile mbingu ikafunuka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutua juu ya ke. Na sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ni Mwanangu, ninayempenda; ni nayependezwa sana" - (Mathayo 3:16,17).

Baada ya kupakwa mafuta kwa Kristo na Roho Mtakatifu wakati ule wa ubatizo wake, wanafunzi wake walitangaza, wakisema:
"Tumemwona Masihi' [Kristo].' - Yohana 1:41.

Wanafunzi wale walijua kwamba neno lile la Kiebrania "Masihi" lilimaanisha "Mpakwa Mafuta."
Luka, mwanafunzi wa Yesu, aliweka katika kumbukumbu zake mwaka wa Yesu aliopakwa mafuta kama Masihi kuwa ulikuwa ni mwaka ule wa kumi na tano wa Kaisari Tiberio (Luka 3:1). Kwetu sisi mwaka ule ungekuwa sawa na mwaka wa 27 B.K.

Zaidi ya miaka 500 kabla ya Kristo kuja hapa, nabii Danieli alitabiri kwamba Yesu angepakwa mafuta kama Masihi katika mwaka ule wa 27 B.K.

"Tangu kutolewa amri ile ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake Mpakwa Mafuta (Masihi)…. Kutakuwa na majuma 'saba' na sitini na mawili jumla yake ni majuma sitini na tisa au siku 483 (7x69= siku 483). Katika mifano ya unabii wa Biblia kila siku ni sawa na mwaka mmoja (Ezekieli 4:6; Hesabu 14:34), hivyo siku hizo 483 ni sawa na miaka 483.

Danieli alitabiri kwamba amri ile ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu ingetolewa katika mwaka ule wa 457 K.K. (Ezra 7:7-26). Kwa hiyo, ile miaka 483 ilikoma katika mwaka ule wa 457 na Kristo alipakwa mafuta mwaka wa 27 B.K., (yote hiyo miwili ikiwa ni sehemu tu ya miaka yenyewe, kwa hiyo, kipindi sahihi kingekuwa miaka 483).

Kwa wakati ule ule hasa uliowekwa katika mwaka ule wa 27 B.K. Yesu alijitokeza akiwa na ujumbe huu:
"Wakati umetimia" (Marko 1:15). Kutimizwa kikamilifu kwa unabii huo wa Biblia ni uthibitisho unaovutia sana unaoonyesha kwamba Yesu wa Nazareti ni Masihi kweli, Mungu katika mwili wa kibinadamu.

Je, ni kwa muda gani Yesu alipaswa kuthibitisha ahadi ile?
"Naye alithibitisha agano [ahadi] thabiti na watu wengi kwa muda wa 'saba' moja [juma, Kiebrania].' - Danieli 9:27, sehemu ya kwanza.

Tunapoitumia kanuni ile ya mwaka mmoja siku moja, basi, "juma" hilo lingekuwa sawa na miaka saba - kuanzia 27 B.K. mpaka 34 B.K - Yesu angeweza ku"lithibitisha agano," au ile ahadi aliyokuwa ameitoa kwa Adamu na Hawa muda mfupi tu baada ya wao kutenda dhambi. Mungu alifanya agano, yaani, ahadi, kwamba angeiokoa jamii ile ya kibinadmu kutoka katika dhambi kwa njia ya yule mmoja ambaye angempeleka ili afe kwa ajili ya dhambi zetu (Mwanzo 3:5).

Je, kungetokea nini katikati ya juma hilo la sabini?
"Katikati ya hiyo "saba" [juma, Kiebrania] atakomesha sadaka na dhabihu." - Danieli 9:27, sehemu ya mwisho.

Yesu alisulibiwa katika mwaka ule wa 31 B.K. "katikati ya juma." Wakati ule wa kifo chake Kristo, Mungu akalipasua "pazia lile la hekalu… likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini" Mathayo 27:51. Mnyama yule wa dhabihu alikuwa karibu kuchinjwa (mfano wa Yesu "Mwana-Kondoo wa Mungu"), akaponyoka mikononi mwa Kuhani. Hii ilikuwa ni ishara iliyoonyesha kwamba Mungu hakutaka wanadamu waendelee tena kutoa dhabihu za wanyama. Unabii ule ukatimizwa neno kwa neno, Yesu "akakomesha na kufanya pasiwe na haja tena ya kutoa dhabihu za wanyama. Tangu kufa kwake Kristo, watu wanamwendea Mungu si kwa njia ya dhabihu za wanyama na makuhani wa kibinadamu, bali kwa njia ya Masihi, Mwana-Kondoo wa Mungu na Kuhani wetu Mkuu.

3. Uhakika Wa Dhambi Zilizosamehewa

Kulingana na unabii wa Danieli, je, kwa nini Yesu alikufa?
"Mpakwa mafuta huyo atakatiliwa mbali, lakini si kwa ajili yake mwenyewe." Danieli 9:26, pambizo.

Alipokufa pale msalabani, Yesu "a[li]katiliwa mbali." Alikufa, "lakini si kwa ajili yake mwenyewe," yaani, si kwa ajili ya kulipa fidia ya dhambi zake mwenyewe, bali kulipa fidia kwa dhambi za ulimwengu mzima.

Sisi twawezaje kujua kwamba Mungu amezisamehe dhambi zetu zote?

"Haki itokayo kwa Mungu huja kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio… WOTE WAMEFANYA DHAMBI…, nao WANAHESABIWA HAKI bure KWA NEEMA YAKE, kwa njia ya ukombozi uliokuja kwa njia ya Yesu Kristo… KWA NJIA YA IMANI KATIKA DAMU YAKE" - (Warumi 3:22-25).

Pointi kuu katika mafungu hayo ni hizi: sisi "[s]ote [tu]mefanya dhambi,'lakini kwa sababu ya "neema," ya Mungu, wote "wanahesabiwa haki" walio na "imani" katika uwezo wa kutakasa wa "damu" yake Kristo. Tunapohesabiwa haki, Mungu anatutangaza sisi kuwa hatuna hatia, anaondoa hatia inayotokana na dhambi zetu zilizopita. Na Mungu kwa njia ya imani katika Yesu Kristo.

Sisi sote tuliochakazwa na jitihada yetu ya kutaka kuwa wema kiasi cha kutosha, ili kukifikia kiwango kile kinachotakiwa kwa kutegemea uwezo wetu wenyewe, tunaweza kupata pumziko la kweli kwa kukubaliwa na Kristo kwa neema yake. Yeye anatuahidi sisi, anasema, "Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha" (Mathayo 11:28). Sisi sote tuliolemewa na mizigo ya makovu tuliyopata zamani, kujiona kuwa hatufai, tena tuna aibu, tunaweza kupata amani na utimilifu ndani ya Kristo.

4. Wakati Wa Hukumu Kuanza

Katika sura ya nane ya Danieli malaika alimwonyesha yule nabii picha kubwa ya matukio ya siku za baadaye. Danieli alimwona (1) Kondoo mume, (2) beberu, na (3) kutoka katika mojawapo ya pembe za yule beberu, "pembe nyingine iliyokuwa ndogo mwanzoni na kukua nguvu zake" (Danieli 8:8,9); mifano hiyo inawakilisha (1)Umedi-Uajemi, (2) Uyunani (Ugiriki), na (3) Roma (Danieli 8:1-12,20-26).

Je, sehemu ya nne ya unabii huo ni ipi?
"Je, itachukua muda gani kwa maono haya kuweza kutimizwa-maono yahusuyo sadaka ya kuteketezwa ya kila siku….? Akaniambia, 'Itachukua jioni na asubuhi 2,300 [au siku, Kiebrania]; ndipo patakatifu patakapowekwa wakfu tena [patakapotakaswa]." - Danieli 8:13,14.

Danieli alizimia kabla yule malaika hajaweza kumweleza sehemu ya siku 2,300 ya unabii ule na sura ya nane inafunga bila kutoa tafsiri yake yote. Lakini baadaye yule malaika alitokea tena na kumwambia hivi:
"Yafahamu maono haya:' Saba' sabini [majuma, Kiebrania] yameamriwa [yamekatwa, Kiebrania] juu ya watu wako na mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu." - Danieli 9:22-24.

Kwa kweli, hizo siku 2,300 ni miaka 2,300, kila siku moja ikiwakilisha mwaka mmoja (Ezekieli 4:6). Majuma sabini, au miaka 490, ilikuwa ndiyo sehemu ya kwanza ya kile kipindi kirefu zaidi cha miaka 2,300. Vipindi vyote viwili vilianza katika mwaka ule wa 457 K.K. wakati Uajemi ilipotoa amri ya "kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu." Miaka ile 490 ikitolewa kutoka katika miaka 2,300, inabaki miaka 12,810. Ikiongezwa miaka hiyo 1,810 kwa mwaka 34 B.K; mwaka ambao miaka ile 490 ilifikia mwisho wake, inatufikisha kwenye mwaka ule wa 1844 B.K.

5. Patakatifu Pa Mbinguni Patakaswa - Hukumu

Malaika yule alimwambia Danieli ya kwamba katika ule mwaka wa 1844, yaani mwisho wa ile miaka 2,300, "patakatifu patatakaswa" (Danieli 8:14, KJV). Lakini hilo maana yake nini? Tangu mwaka wa 70 B.K. Waroma walipoliteketeza hekalu kule Yerusalemu, watu wa Mungu hawana hekalu lo lote hapa duniani. Kwa hiyo patakatifu patakapotakaswa kuanzia ule
mwaka wa 1844 ni lazima pawe ni pale patakatifu pa mbinguni ambapo hekalu lile la duniani lilikuwa nakala yake halisi.

Haya! Kutakaswa kwa patakatifu pale pa mbinguni maana yake ni nini? Israeli ya zamani iliita siku ile ya kupatakasa patakatifu pa kidunia Yom Kippur, yaani, Siku ya Upatanisho. Kwa kweli ile ilikuwa ni Siku ya HUKUMU.

Kama tulivyogundua katika Mwongozo 12, kazi ile anayofanya Kristo kwa ajili yetu katika patakatifu pale ina awamu mbili: (1) Dhabihu za kila siku ambazo hulenga ile huduma ya Kuhani katika chumba kile cha kwanza cha Patakatifu. (2) Dhabihu ya kila mwaka ambayo inaitilia nguvu huduma ya Kuhani Mkuu katika chumba kile cha pili, yaani, Patakatifu pa Patakatifu ( Walawi 16).

Katika lile hekalu la kidunia, watu walipoziungama dhambi zao siku kwa siku, damu ya wanyama wale waliochinjwa ilimwagwa kwenye pembe ya madhabahu ile, kisha ilihamishiwa katika Patakatifu (Mambo ya Walawi 4 na 6). Hivyo, kwa mfano, siku baada ya siku dhambi zilizoungamwa ziliingizwa ndani ya Patakatifu na kuwekwa pale.

Halafu, kila mwaka, katika ile Siku ya Upatanisho, patakatifu pale palitakaswa kutokana na dhambi zote zilizoungamwa katika kipindi cha mwaka uliopita (Mambo ya Walawi 16). Ili kufanya utakaso huo, Kuhani Mkuu alitoa sadaka maalum ya mbuzi aliyewekwa wakfu. Kisha aliichukua damu yake na kuingia nayo mpaka Patakatifu pa Patakatifu na kuinyunyiza damu ile ya utakaso mbele ya kile kifuniko cha upatanisho [kiti cha rehema] ili kuonyesha kwamba damu ya Yesu, Mkombozi aliyekuwa anakuja, ingeweza kulipa fidia ya dhambi ile. Kisha kwa mfano yule Kuhani Mkuu aliziondoa dhambi zile zilizoungamwa kutoka patakatifu pale na kuziweka juu ya kichwa cha mbuzi yule mwingine, ambaye alipelekwa mbali katika jangwa na kuachwa afe kule (Mambo ya Walawi 16:20-22).

Taratibu hiyo ya ibada iliyofanywa kila mwaka katika siku ya upatanisho ilipatakasa pale patakatifu kutokana na dhambi. Watu waliiona kuwa ilikuwa ni siku ya hukumu kwa kwa sababu wale waliokataa kuziungama dhambi zao walifikiriwa kuwa ni waovu, nao "walikatiliwa mbali na watu wake [Mungu]" (Mambo ya Walawi 23:29).

Alichofanya kwa mfano, yule Kuhani Mkuu, mara moja kwa mwaka, Yesu anafanya mara moja kwa wakati wote akiwa Kuhani wetu Mkuu (Waebrania 9:6-12). Katika siku hii kuu ya hukumu yeye anaziondoa kutoka katika patakatifu dhambi zile zilizoungamwa za wale wote waliompokea kama Mwokozi wao. Kama sisi tumeziungama dhambi zetu, basi, yeye ataifuta kumbukumbu ya dhambi zetu wakati ule (Matendo 3:19). Huduma hiyo ni kazi ya hukumu ambayo Yesu aliianza katika mwaka ule wa 1844.

Katika mwaka wa 1844 saa ya hukumu ilipoanza kule mbinguni ujumbe wa saa ya hukumu imekuja ulianza kuhubiriwa ulimwenguni kote (Ufunuo 14:6-7). GUNDUA Mwongozo baadaye litaushughulikia ujumbe huo.

6. Kukabiliana Na Kumbukumbu Ya Maisha Yako Hukumuni

Tangu mwaka wa 1844 Kristo, kama Jaji, amekuwa akiichunguza kumbukumbu ya kila mmoja aliyepata kuishi ili kuthibitisha ni akina nani watakaokuwamo miongoni mwa wale watakaookolewa Yesu atakapokuja. Kama Jaji wetu, Yesu "anazifuta" dhambi zote za wenye haki kutoka katika kumbukumbu zao za maisha zilizoko kule mbinguni (Matendo 3:19).

Jina lako linapoitwa katika hukumu hiyo, itakuwa rahisi kwako kukabiliana na kumbukumbu ya maisha yako - ENDAPO wewe utakuwa umempokea Kristo kama mbadala wako. Na hukumu ya wenye haki itakapokwisha, Yesu atarudi duniani kuwalipa ujira wao (Ufunuo 22:12,14).

Je! hivi wewe u tayari Yesu akija? Au, je! kuna kitu fulani ambacho umekuwa ukimficha? Je! unao uhusiano huru na wa kweli na yule Mmoja anayetoa ahadi hii:
"Tukiziungama dhambi zetu yeye ni mwaminifu na wa haki, hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha udhalimu wote." - 1 Yohana 1:9.

Ungamo maana yake rahisi ni kukubali kukabiliana na dhambi zetu, kupokea msamaha wa Mungu, na kukiri kwamba tunahitaji uweza wake na neema yake.

Alipokuwa akilitembelea gereza moja katika mji wa Potsdam, mfalme Frederick William alisikiliza maombi kadhaa ya msamaha. Wafungwa wote waliapa kwamba Majaji wale walipendelea, mashahidi walikuwa wa uongo, au wanasheria walikuwa si wanyofu ambao walihusika na kifungo chao. Toka seli hata seli kisa kile kile cha kutendewa vibaya, wao wakiwa hawana hatia, kiliendelea kusimuliwa.

Lakini katika seli moja mfungwa mmoja hakuwa na la kusema. Akiwa ameshangaa, Frederick akamtania, "Nadhani na wewe pia huna hatia yo yote."
"Hasha, mfalme," yule mtu alijibu, "Mimi nina hatia, tena nastahili kabisa yote ninayopata."

Mfalme akamgeukia mlinzi na kumwita kwa sauti kuu, "Njoo umwachilie upesi mhuni huyu kabla hajaliharibu kundi hili zuri la watu wasio na hatia yo yote."

Je! tunajiandaaje kwa hukumu hiyo? Tunajiwekaje tayari kwa ajili ya kuja kwake Kristo? Kwa kuikiri kweli peke yake kwa moyo mnyofu: Mimi nastahili kabisa adhabu ya kifo kwa dhambi zangu, lakini yule mwingine amechukua mahali pangu na kunipa msamaha wake wa ajabu.

Amua sasa hivi kwamba chochote kile kinachotokea, wewe utadumisha uhusiano wako na Kristo ukiwa unatazamana naye jicho-kwa-jicho kwa unyofu wa moyo-kwa-moyo kwa uaminifu.


© 2004 The Voice of Prophecy Radio Broadcast
Los Angeles, California, U.S.A.