KUHUSU MAMBO YAKO YA BAADAYE

Madaktari Patricia na David Mrazek walikuwa wamelemewa na huzuni kubwa sana katika kazi yao. Kama mabingwa wa magonjwa ya watoto, waliwashughulikia watoto wengi waliokuwa wakiumwa. Lakini waligundua ukweli kwamba baadhi ya watoto walitoka katika hatari yao ya kufisha na kupata nguvu mpya, ambapo wengine waliangamizwa nayo. Kwa nini? Mathalani, kwa nini mtoto mmoja atumie madawa ya kulevya wakati yule mwingine anakwenda kusoma chuoni? Kwa nini baadhi ya watoto waliotendewa vibaya wanakua na kujitendea vibaya wenyewe, wakati wengine wanakuwa wazazi wazuri?

Akina Mrazek hao walifanya utafiti wao mpana sana ili kupata majibu kwa maswali hayo. Katika uchunguzi wao tabia moja iliyozidi zote ilizidi kujitokeza miongoni mwa watoto wale walionusurika kutoka katika kiwewe chao na kuendelea kuwa na maisha "ulikuwa ni ule mtazamo wa maisha uliojengwa juu ya mwelekeo wa kutazamia kuyaona mambo mazuri siku za mbele na kuwa na matumaini."

Kuwa na tumaini kulileta tofauti ile. Tumaini, kuliko kitu kinginecho chote, linatusaidia sisi kuyashinda mambo ya ajabu-ajabu yanapokuja kwa wingi sana dhidi yetu.

Wanadamu wanalihitaji tumaini sana. Lakini, je! tunalipataje? Tumaini katika ulimwengu wetu huu ni vigumu kuliona - MPAKA tuliangalie kwa mtazamo wa unabii wa biblia. Mwongozo huu wa GUNDUA unauchunguza unabii ule wa maana sana uliowatia tumaini lenye nguvu watu wengi wasio na idadi.

1. Unabii wa Biblia Unaoshangaza

Karibu miaka mia tano hivi kabla ya kuzaliwa kwake Kristo, Mungu aliupa ulimwengu huu mtazamo wa haraka wa mambo ya mbele unaoshangaza sana kupitia kwa nabii Danieli. Mungu alitoa muhtasari wa historia ya ulimwengu huu miaka 2,500 kabla ya kutokea, kuanzia wakati ule wa Danieli mpaka siku zetu hizi.

Unabii huo ulianzia katika ndoto ambayo Mungu alimpa Nebukadreza, Mfalme wa Babeli, yapata mika 2,500 hivi iliyopita. Ndoto ile ilimsumbua sana mfalme yule - lakini hakuweza kuikumbuka ndoto ile alipoamka kutoka usingizini! Baada ya wenye hekima wote wa Babeli kushindwa kumsaidia mfalme yule kuikumbuka ndoto yake au kuifasiri, kijana mmoja Mwebrania, aliyekuwa kule uhamishoni, kwa jina Danieli, alijitokeza kwenye mandhari ile, akidai kwamba Mungu wa Mbinguni alikuwa na uwezo wa kuzifunua siri zote.

Akiwa amesimama mbele ya mfalme yule, akanena kwa ujasiri, akasema "Wewe, Ee, mfalme, ulitazama, na pale mbele yako ilisimama SANAMU KUBWA - sanamu kubwa sana, inayong'aa.
"Kichwa cha sanamu ile kilitengenezwa kwa dhahabu safi, kifua na mikono yake ni ya fedha, tumbo lake na mapaja yake ni ya shaba nyekundu, miguu yake ni ya chuma, na nyayo zake nusu za chuma na nusu za udongo wa mfinyanzi uliochomwa.
"Ulipokuwa ukiangalia, jiwe lilichongwa, lakini si kwa mikono ya wanadamu. Likaipiga ile sanamu katika nyayo zake za chuma na udongo na kuivunja vipande vipande.
"Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba nyekundu, na ile fedha, na ile dhahabu, vikavunjwa vipande vipande wakati ule ule na kuwa kama makapi juu ya sakafu ya kupepetea wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha mbali bila kuacha kitu cho chote mahali pake. Lakini ULE MWAMBA ULIOIGONGA SANAMU ILEukawa mlima mkubwa, UKAIJAZA DUNIA YOTE" - (Danieli 2:31-35).

Sanamu hiyo, kwa kuitupia jicho mara moja, yaweza kuonekana kana kwamba haina kazi sana kuweza kutupatia sisi tumaini katika nyakati hizi tunazoishi, lakini wewe endelea tu kusoma habari zake.

2. Unabii Watafsiriwa

Baada ya kumsimulia Nebukadreza aliyekuwa amevutiwa sana na kile alichokuwa amekiona hasa katika maono yake, nabii Danieli alitoa ufafanuzi wake:
"Hii ndiyo ile ndoto, na sasa tutaifasiri kwa mfalme" - (Danieli 2:36).

KICHWA CHA DHAHABU: Je, ni mamlaka gani ya dunia ambayo Danieli alimwambia yule mfalme kuwa ilionyeshwa kwa mfano wa kichwa cha dhahabu?
"Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe ufalme na uwe, na nguvu, na utukufu.... WEWE U KICHWA KILE CHA DHAHABU" - mafungu ya 37,38).

Danieli alikuwa anampasha habari hizi mtawala yule wa dola kubwa kuliko zote ulimwenguni: "Nebukadreza, Mungu anakuambia wewe kwamba dola yako, Babeli, imewakilishwa na kichwa hicho cha dhahabu cha hiyo sanamu."

KIFUA NA MIKONO YA FEDHA. Kwa mtazamo wa kibinadamu Babeli ilionekana kama dola ambayo ingeweza kudumu milele. Lakini, je, unabii unasema kitu gani kitatokea baada yake?
"Baada yako, utainuka ufalme ulio mdogo kuliko wako" fungu la 39.

Kwa kutimiza utabiri huo wa Mungu, ufalme ule wa Nebukadreza ulivunjika vipande vipande na kuwa magofu wakati yule Koreshi, Jemedari wa Kiajemi,
alipoiangusha dola ile ya Babeli mwaka ule wa 539 K.K. kwa hiyo, kifua na mikono ya fedha huwakilisha Uamedi na Uajemi, dola nyingine yenye nguvu nyingi.

TUMBO NA MAPAJA YA SHABA NYEKUNDU: Sehemu hii ya sanamu ile kubwa ya madini huwakilisha nini?
"Halafu, ufalme wa tatu, ufalme wa shaba nyekundu, utatawala juu ya ulimwengu nzima." - (fungu la 39).

Tumbo na mapaja ya shaba nyekundu ni mfano wa ufalme wa Uyunani (Ugiriki). Iskanda mkuu (Alexander the Great) aliwashinda Waamedi na Waajemi, na kuingiza Uyunani kuwa dola kuu ya tatu ya ulimwengu . ilitawala kuanzia mwaka wa 331 hadi mwaka 168 K.K.

MIGUU YA CHUMA:
"Hatimaye, patakuwa na ufalme wa nne [alisema yule nabii], wenye nguvu kama chuma - kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kukishinda kila kitu - na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta zile nyingine zote." -(fungu la 40).

Baada ya kifo chake Iskanda, dola yake ilidhoofika na kugawanyika katika makundi yanayoshindana mpaka hatimaye katika mwaka ule wa 168 K.K, "Dola ya Chuma" ya Roma ikaishinda Uyunani katika vita ya Pydna.

Kaisari Augusto alitawala katika ile Dola ya Roma wakati alipozaliwa Yesu mnamo miaka elfu mbili iliyopita (Luka 2:1). Kristo na mitume wake waliishi katika kipindi kile kilichowakilishwa na miguu ya chuma. Giboni, mwanahistoria wa karne ile ya kumi na nane, bila shaka mawazoni mwake alikuwa na unabii wa Danieli, alipoandika maneno haya: "Zile sanamu za dhahabu, au fedha, au shaba, ambazo zingetumika kuyawakilisha mataifa na wafalme wao, zilivunjwa na kurithiwa na ufalme ule wa chuma wa Roma" - Edward Gibbon, The History of the Decline and Fall of the Roman Empire (John D. Morris and Company), gombo la 4, uk. 89.

Hebu kwa dakika moja tafakari juu ya utabiri huo kwa mtazamo wa kibinadamu. Je, kwa vipi Danieli, aliyeishi katika kipindi kile cha Babeli, angekuwa na wazo lo lote kuhusu dola ngapi zingefuatana moja baada ya nyingine mamia ya miaka katika siku zile za mbele. Sisi tunakuwa na wakati mgumu kukisia soko la biashara litakuwaje juma lijalo! Na, hata hivyo, Babeli, Umedi-Uajemi, Uyunani, na Roma zilifuatana kabisa moja baada ya nyingine, kama vile ilivyotabiriwa - kama watoto wa shule watiifu ambao wamesimama katika mstari.

Je, Mungu anayadhibiti mambo yale ya baadaye? Je, tunaweza kuwa na tumaini kwa kutegemea msingi wa mpango wake ule mkuu? Jibu lake ni "Ndiyo!" ivumayo kote.

NYAYO NA VIDOLE VILIVYOCHANGANYIKA CHUMA NA UDONGO:
Je! kuna dola ya tano ya ulimwengu mzima ambayo ingefuata baada ya Roma?
"Na kama vile ulivyoziona nyayo na vidole vyake kuwa vilikuwa nusu udongo na nusu chuma, hivyo HUO UTAKUWA NI UFALME ULIOGAWANYIKA; hata hivyo, utakuwa na nguvu kiasi fulani za chuma ndani yake, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa mfinyanzi. Na chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu na nusu yake umevunjika" - (Danieli 2:41,42).

Nabii huyo alitabiri, sio juu ya dola ya tano ya ulimwengu mzima, bali juu ya mgawanyiko wa ufalme ule wa chuma wa Roma. Roma ingevunjika katika falme kumi, kama ilivyowakilishwa na nyayo na vidole vya ile sanamu.

Je, jambo hilo lilitokea kweli? Hakika lilitokea. Katika kipindi cha karne ile ya nne na ya tano ya kipindi kile cha Kikristo washambuliaji wa kishenzi (wasiostaarabika) kutoka kaskazini walimiminika kushuka chini kuja katika Dola ya Kiroma iliyokuwa inazidi kupungua nguvu zake, wakaipiga kipigo baada ya kipigo. Hatimaye kumi miongoni mwa makabila yale yakajipatia sehemu kubwa ya Roma ya Magharibi, na mataifa kumi tofauti yanayojitawala yenyewe yakajiimarisha katika mipaka ile ya Ulaya. Hivyo vidole vile leo vinayawakilisha mataifa ya siku hizi ya Ulaya.

Vidole Kumi - Makabila Makuu Kumi Katika Dola Ya Roma Ya Magharibi
Anglo - Saxons Uingereza
Franks Ufaransa
Alemanni Ujerumani
Lombards Italia
Ostrogoths Wagothi wa Mashariki waliangamizwa baadaye
Visigoths Wagothi wa Magharibi au Hispania
Burugundians Uswis - Switzerland
Vandals Wavandali - Afrika Kaskazini,
waliangamizwa baadaye
Suevi Ureno
Heruli Waharuli - walitoweka baada ya karne chache tu

4. Mtazamo katika Wakati Ujao

Sehemu moja tu ya unabii wa Danieli bado haijatimizwa. Jiwe lile, je! linamaanisha nini ambalo linaipiga ile sanamu nyayoni, na kuisaga tikitiki, kasha ligeuka na kuwa mlima mkubwa unaoijaza dunia nzima?

"KATIKA SIKU ZA WAFALME HAO [mataifa ya siku hizi ya Ulaya (Magharibi)]. MUNGU WA MBINGUNI ATAUSIMAMISHA UFALME ambao hautaangamizwa kamwe, wala watu wengine hawataachiwa. Utazivunja falme hizo zote vipande vipande na kuzikomesha, lakini WENYEWE UTADUMU MILELE NA MILELE" - (Danieli 2:44).

"Wafalme hao" huwahusu tu wafalme wale waliowakilishwa na nyayo na vidole vya sanamu ile - yaani, watawala wa Ulaya (Magharibi) ya leo, huzionyesha siku zetu. Jiwe lile lililochongwa bila kutumia mikono ya kibinadamu litaipiga hiyo sanamu na kuivunja vipande vipande, kisha litaijaza dunia nzima (mafungu ya 34, 35, 45). Yesu atashuka hivi karibuni kutoka mbinguni kuja ku "usimamisha ufalme," huo, yaani, ufalme wake uliojaa furaha na amani. Hapo ndipo Kristo, Mwamba wa Kale na mfalme wa wafalme, atakapoitwaa dunia hii milele hata milele!

Kila kitu katika utabiri wa Danieli 2 kimetimia isipokuwa lile tendo la mwisho yaani, kupigwa kwa sanamu hiyo na lile jiwe. Kulingana na ratiba ya Mungu, hivi sasa tunakikaribia kilele kile kikuu, yaani, kurudi kwake Kristo katika dunia yetu. Yesu Kristo, Mwana wa Mungu yu karibu sana kulikomesha hilo pambano la umwagaji wa damu la muda mrefu katika historia ya kibinadamu na kusimamisha ufalme wake wa milele wa upendo na neema.

5. Ndoto Ya Mfalme Na Wewe

Unabii huu hudhihirisha mkono wa Mungu uongozi katika kuinuka na kuanguka kwa mataifa. Mungu anajua yaliyopita, na huo unabii wa Biblia huonyesha wazi kwamba yeye anajua mambo ya baadaye pia.

Kama Mungu anaongoza nyendo za mataifa kwa usahihi mkamilifu kama huo, basi, ni hakika kwamba anaweza kuyaongoza maisha ya kila mtu mmoja mmoja. Yesu alituhakikishia sisi kwamba: "Hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi" (Mathayo 10:30-31). Zawadi ya Mungu ya imani inaweza kuwa dawa ya kupunguza wasi wasi na hofu zetu zote. Tumaini analoliamsha ndani yetu linaweza kuwa nanga ya roho zetu (Waebrania 6:19).

Erasmo, mtaalam wa Biblia wa karne ya kumi na sita, alisimulia habari za tukio moja lililotokea wakati wa safari yake baharini, ambayo ilichukua maisha yake yote. Chombo alichokuwa anasafiria kilipwelea wakati wa dhoruba. Mawimbi yenye nguvu yakakipiga, kikaanza kupasuka, hata mabaharia walianza kuingiwa na hofu kuu. Abiria walikuwa karibu kupagawa.

Wengi sana walipiga makele wakiomba msaada toka kwa mtakatifu wao mlezi, waliimba nyimbo za kumsifu Mungu, au walimsihi sana Mungu kwa sauti kuu katika sala zao.

Walakini, Erasmo alimgundua abiria mmoja aliyekuwa tofauti. "Miongoni mwetu sisi sote, "aliandika Erasmo, "yule aliyebaki akiwa ametulia karibu kabisa alikuwa ni mwanamke mmoja kijana aliyekuwa amempakata mtoto wake mchanga aliyekuwa akiendelea kumnyonyesha. Yeye peke yake ndiye hakupiga makelele, hakulia, wala kujaribu kupatana na mbingu. Hakufanya kitu kingine cho chote, bali aliomba kimya kimya moyoni mwake huku akiendelea kumshikilia sana mtoto wake yule mchanga kwenye paja lake."

Saa ile, Erasmo alitambua, ilikuwa ni kuendelea na maisha yake ya sala ya kila siku. Alionekana kana kwamba amejikabidhi mwenyewe kwa Mungu.

Meli ile ilipoanza kuzama, mama yule kijana aliweka juu ya ubao, na kupewa mhimili wa kutumia kama kasia kisha akaachiwa apate kukabiliana na yale mawimbi. Akalazimika kumshika mtoto wake kwa mkono mmoja na kujaribu kupiga kasia kwa mkono ule mwingine. Ni wachache mno waliodhani kwamba atanusurika katika mawimbi yale yaliyokuwa yameumuka.

Lakini imani yake na ule utulivu wake ulimweka katika hali nzuri. Yule mwanamke na mtoto wake walikuwa wa kwanza kufika pwani.

Tumaini kwa Mungu aliye mwaminifu linaweza kuleta tofauti kubwa sana - hata dunia yetu hii inapoonekana kana kwamba inapasuka pande zote kutuzunguka. Sisi hatuko kule nje kupiga kasia kwa kujitegemea wenyewe. Mkono mkubwa zaidi unatuongoza na kutushika.

Ukija kwa Kristo kwa kujitoa kwake kabisa, atakupa imani ambayo itakupitisha salama katika kila dhoruba. Gundua amani hii ipitayo ufahamu wote ambayo Yesu anakuahidi kukupa:
"Amani nawachieni, amani yangu nawapa….. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga" - (Yohana 14:27.

Je! unayo amani hiyo? Kama unayo, basi, mshukuru Yesu, Mwokozi wako. Kama hunayo, kwa nini usimkaribishe katika maisha yako leo hii?


© 2004 The Voice of Prophecy Radio Broadcast
Los Angeles, California, U.S.A.