JE! MAISHA YANGU YANA MAANA KWA MUNGU?

1. Mungu Aliumba Dunia Kamilifu

Mungu ndiye Muumbaji, mwasisi na mbunifu wa kila kitu kuanzia nyota zinazotoa mlipuko wa mwanga mkubwa kuliko jua na kutoweka (supernovas) hadi mabawa ya kipepeo.

"Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.... maana yeye alisema, ikawa; na yeye aliamuru, ikasimama" - (Zaburi 33:6-9).

Mungu hana budi kusema tu, kisha vitu vya asili hutii mapenzi yake.

2. Siku Sita Kuifanya Dunia Yetu

"Kwa siku zita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba. Kwa hiyo, BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa" - (Kutoka 20:11).

Muumbaji huyo wa milele, mwenye uweza wote angeweza kuiumba dunia hii kwa dakika moja "kwa pumzi ya kinywa chake." Lakini Mungu alichagua kuchukua siku sita kufanya kazi hiyo dakika sita, au hata nukta sita zingekuwa zinatosha. Sura ile ya kwanza katika Biblia, yaani, Mwanzo 1, inaeleza kile Mungu alichokiumba katika kila siku ya juma lile la Uumbaji.

Ni kazi gani bora ya kilele aliyoiumba Mungu katika siku ile ya sita?
"Mungu Akaumba Mtu Kwa Mfano Wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba; Mwanaume Na Mwanamke Aliwaumba" - (Mwanzo 1:27).

Juma La Uumbaji
Siku ya Kwanza: Nuru; mfuatano wa mchana na usiku
Siku ya Pili: Anga, hewa ya dunia hii
Siku ya Tatu: Nchi kavu na mimea
Siku ya Nne: Jua na mwezi vikaonekana
Siku ya Tano: Ndege na Samaki
Siku ya Sita: Wanyama wa nchi kavu na mwanadamu
Siku ya Saba: Sabato

Mungu aliamua kuwaumba watu wanaofanana naye ambao wangeweza kufikiri na kujisikia na kupenda. Kila mtu ameumbwa kwa "mfano" wa Mungu.

Kufikia siku ile ya sita, dunia hii ilikuwa imejazwa na mimea na wanyama, ndipo Mungu akaileta kazi yake bora kuliko zote ya uumbaji. Kulingana na Mwanzo 2:7, Mwenyezi aliuumba mwili wa Adamu kwa mavumbi ya ardhi. Basi Mungu alipompulizia "pumzi ya uhai", puani mwake, mtu akawa "kiumbe hai" - yaani, akawa na uhai. Mungu alimwita Adamu, yule mtu wa kwanza aliyeumbwa kwa mfano wake, neno hilo limaanishalo tu "mtu" na mwanamke yule wa kwanza akamwita Hawa maana yake, "aliye hai" (2:20; 3:20). Muumbaji huyo mweye upendo aliona ipo haja kwa binadamu kuwa na mwenzi.

Wakiwa wametoka wenye afya mkononi mwake Mungu, Adamu na Hawa, wote wawili, waliakisi [walirudisha mwanga wa] sura yake. Mungu angeweza kuwaumba wanadamu kama [kikaragosi] roboti wakizurura huku na huku katika ile bustani ya Edeni na kutosheka na kupaza sauti zao kumwabudu yeye. Lakini Mungu alitaka zaidi ya hilo; yaani, alitaka kuwa na uhusiano wa kweli nao. Maroboti yanaweza kutabasamu, kusema, na hata kuosha vyombo vya kulia chakula, ila hayawezi kupenda.

Mungu alituumba sisi kwa mfano wake, tukiwa na uwezo wa kufikiri na kuchagua, na kukumbuka, kufahamu na kupenda. Adamu na Hawa walikuwa watoto wa Mungu, na kwa namna isiyoelezeka walikuwa wanapendwa sana naye.

3. Uovu Waingia Katika Dunia Hii Kamilifu

Adamu na Hawa walikuwa na kila kitu cha kuwaletea furaha. Walifurahia kuwa na afya kamili kimwili na kiakili, wakiishi katika bustani ile nzuri katika dunia hii isiyo na dosari (Mwanzo 2:8; 1:28-31). Mungu aliwaahidi kuwapa watoto na kufurahia kuona kazi ya mikono yao (Mwanzo 1:28; 2:15). Walikuwa na uzoefu wa kirafiki wa ana kwa ana na Muumbaji wao. Hapakuwa na wasiwasi, hofu, au ugonjwa wo wote wa kuziathiri siku zao zilizowaletea furaha kamili.

Je, dunia hii ilibadilikaje kwa ghafula mno na kuwa mahali pa mateso na misiba? Sura ya pili na ya tatu ya Mwanzo inatusimulia kisa chote juu ya jinsi dhambi ilivyoingia katika dunia yetu. Uzisome kwa nafasi yako. Hapa ni muhtasari mfupi wa mambo yaliyomo katika sura hizo.

Muda fulani baada ya Mungu kuiweka dunia hii kamilifu, yule Shetani akaja katika Bustani ile ya Edeni kumjaribu Adamu na Hawa ili wamwasi Muumbaji wao. Mungu alimwekea yule Shetani mipaka ya mvuto wake kwenye mti mmoja tu katika ile bustani, yaani, kwenye ule "mti wa ujuzi wa mema na mabaya." Kisha akawaonya wale watu wawili, mume na mke, kuwa mbali na mti ule na kutokula kabisa matunda yake, la sivyo, wangekufa.

Lakini siku moja Hawa akazurura kuelekea karibu na mti ule uliokatazwa. Shetani akamshambulia upesi kwa kumwuzia maneno ya kumshawishi. Alidai kwamba Mungu alikuwa amesema uongo kwake na ya kwamba endapo yeye angekula matunda ya mti ule, asingekufa, ila angekuwa na hekima kama Mungu mwenyewe, akijua mema na mabaya. Kwa bahati mbaya sana Hawa, na hatimaye Adamu, ambao walikuwa wanayajua mema tu, wakamruhusu Shetani kuwarubuni, kisha wakalionja lile tunda lililokatazwa - hivyo kukivunja kifungo chao cha imani na utii kwa Mungu.

Mungu alikuwa amefanya mpango kwamba Adamu na Hawa wa "tawale" dunia yetu hii kama mawakili wake wa kazi zile alizoziumba Mungu (Mwanzo 1:26). Lakini kwa kuwa walikosa uaminifu kwa Mungu na kumchagua Shetani kama kiongozi wao mpya, basi, wale watu wawili, mume na mke, wakaipoteza mamlaka yao. Leo hii Shetani anadai kwamba dunia hii ni yake, tena anajitahidi sana kuwanasa watu wa dunia hii.

Mara nyingi sana tunajikuta tukifanya jambo fulani la uchoyo au hata kuwa wakatili wakati tunalotaka kufanya hasa ni kinyume chake. Hivi kwa nini? Kwa sababu huyo adui asiyeonekana kwa macho yetu, yaani, huyo Shetani, anafanya kazi yake ili kuwafanya watu washindwe kimaadili.

Unapoisoma sura ya tatu ya Mwanzo, utagundua kwamba dhambi ilimfanya Adamu na Hawa kujificha kwa hofu ili Mungu asiwaone. Dhambi iliathiri uumbaji wote. Miiba ikajitokeza pamoja na maua. Ardhi ikaathirika kwa ukame, na kazi ikawa ni mzigo ulemeao. Ugonjwa ukaanza kuwashambulia watu hapa na pale bila kuwa na mpangilio. Wivu chuki, na uchoyo vikazidisha taabu zao. La kutisha mno, pamoja na ile dhambi ikaja mauti.

4. Shetani Huyo Ni Nani Ambaye Aliiambukiza Dunia Yetu Dhambi?

"Yeye alikuwa MWUAJI TANGU MWANZO; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, yaliyo yake mwenyewe, kwa sababu yeye ni mwongo na BABA WA UONGO" - (Yohana 8:44).

Kulingana na Yesu, Shetani ndiye mwanzilishi wa dhambi katika dunia hii, yeye ni "baba" wa dhambi na hivyo ni baba wa mauaji na uongo

Thomas Carlyle, mwanafalsafa mashuhuri wa Kiingereza, siku moja alimchukua Ralph Waldo Emerson na kumtembeza kupitia katika baadhi ya mitaa michafu sana iliyoishia mashariki mwa mji wa London. Walitembea pamoja, wakiangalia kimya kimya na kuona umaskini na uovu uliowazunguka pande zote, hatimaye Carlyle akauliza, "Je! unaamini juu ya Shetani sasa?"

5. Je! Mungu Alimwumba Shetani?

La! Mungu mwema asingeweza kumwumba Shetani. Na, hata hivyo, Biblia inasema kwamba Shetani, pamoja na malaika wale aliowadanganya, walipoteza mahali pao mbinguni na kuja katika dunia yetu.

"Kulikuwa na VITA MBINGUNI. Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, naye JOKA NA MALAIKA ZAKE akapigana nao. Nao hawakushinda wala mahali pao hapakuonekana mbinguni. Yule joka mkubwa akatupwa chini kwa nguvu - nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, audanganyaye ulimwengu wote. Akatupwa kwa nguvu mpaka duniani, na malaika zake wakatupwa pamoja naye" (Ufunuo 12:7-9).

Huyo Shetani aliingiaje kwanza kule mbinguni?

"Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye. Naam nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu;...... ULIKUWA MKAMILIFU KATIKA NJIA ZAKO tangu siku ile ULIPOUMBWA HATA UOVU ULIPOONEKANA NDANI YAKO" (Ezekieli 28:14,15).

Mungu hakumwumba Shetani, alimwumba Lusifa, malaika mkamilifu, mmojawapo wa malaika wakuu wa mbinguni, aliyesimama karibu na kiti cha enzi cha Mungu. Lakini baadaye alitenda dhambi -"uovu ulionekana ndani" yake. Akiwa amefukuzwa mbinguni, naye akijifanya ni rafiki wa Adamu na Hawa, aligeuka na kuwa adui, mwenye madhara makubwa mno, kwa wanadamu.

6. Kwa Nini Lusifa, Alitenda Dhambi?

"Jinsi ULIVYOANGUKA KUTOKA MBINGUNI, Ewe nyota ya alfajiri (Lusifa), mwana wa asubuhi!........ Nawe ulisema moyoni mwako, "Nitapanda mpaka mbinguni; nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu.......... NITAFANANA NA YEYE ALIYE JUU"- (Isaya 14:12-14).

Kiumbe yule aliyegeuka na kuwa Shetani, zamani aliitwa Lusifa, maana yake "nyota ya alfajiri" au "yule anayeng'aa." Ndani ya moyo wa malaika huyo, kiburi na kutaka makuu, mambo hayo, yakaanza kuchukua mahali pa kumwabudu Mungu. Mbegu ya kiburi ikakua mpaka ikawa tamaa isiyotulizika ya kutaka kuchukua mahali pa Mungu.

Bila shaka Lusifa alikuwa amejitahidi sana kuwashawishi viumbe wale wengine wa mbingu. Ni rahisi kuingiwa na mawazo na kumwona Shetani akibishana na Mungu kwamba alikuwa akizuia kitu fulani ili wao wasikipate, na ya kwamba sheria ya Mungu [Amri Kumi] ilikuwa inawabana vibaya mno, na ya kwamba Mungu alikuwa ni mtawala asiyejali. Akamsingizia yule mmoja ambaye tabia yake inaonyesha upendo ni nini.

Vita hiyo ilisuluhishwaje kule mbinguni?
"Moyo wako ukiinuka kwa sababu ya uzuri wako,........... nimekutupa chini" (Ezekieli 28:17).

Kiburi kilimgeuza yule mkuu wa malaika na kumfanya Ibilisi au Shetani. Na ili kuhifadhi amani na umoja ulioko kule mbinguni, yeye pamoja na theluthi moja ya malaika wa mbinguni waliojiunga naye katika maasi yale. Wakapaswa kufukuzwa kule (Ufunuo 12:4, 7-9).

7. Nani Anawajibika Kwa Dhambi?

Kwa nini Mungu hakuwaumba viumbe wasio na uwezo wa kutenda dhambi? Kama angefanya vile, basi, pasingekuwako na tatizo lo lote la uovu katika dunia yetu. Lakini Mungu alitaka kuwa na watu ambao wangekuwa na uhusiano unaoleta maana. Kwa hiyo "Mungu akaumba mtu kwa mfano wake" (Mwanzo 1:27). Hii maana yake ni kwamba sisi tuko huru, tena tunawajibika. Tunaweza kuamua kumpenda Mungu au kumgeuzia migongo yetu.

Mungu aliwapa malaika wale pamoja na wanadamu wa kila kizazi, tabia ya kiroho na uwezo wa kufanya tabia ya kiroho na uwezo wa kufanya uchaguzi halisi.

"Chagueni wenyewe hivi leo mtakayemtumikia." Yoshua 24:15.

Mungu anatoa changamoto kwa viumbe wake aliowaumba kwa mfano wake ili wachague kutenda mema kwa sababu uwezo wao wa kufikiri unawaambia kwamba "Njia ya Mungu ni bora kuliko zote." Kisha kugeukia mbali na makosa kwa sababu uwezo wao wa kufikiri unawaonya dhidi ya matokeo ya uasi na dhambi.

Ni viumbe wale tu walio na uwezo wa kufikiri na kuchagua wawezao kuwa na upendo wa kweli. Mungu alitamani sana kuwaumba watu ambao wangeweza kuijua na kuithamini tabia yake, kuitikia kwa kuonyesha upendo wao kwake, na kujazwa na upendo wake, kwa ajili ya wengine. Mungu alitaka sana kuwashirikisha upendo wake hata akawa tayari kujiingiza katika hatari kubwa mno ya kuwaumba malaika na wanadamu wenye uwezo wa kuchagua. Alijua kwamba uwezekano uliokuwapo kwamba siku moja mmojawapo wa viumbe wake aliowaumba angeweza kuchagua asimtumikie yeye. Shetani alikuwa kiumbe wa kwanza katika malimwengu kufanya uchaguzi wa kutisha. Misiba iliyoletwa na dhambi ilianzishwa naye (Yohana 8:44, 1 Yohana 3:8).

8. Msalaba Unafanya Uwezekano Uwepo Wa Kuangamizwa Kwa Dhambi

Kwa nini Mungu hakumwangamiza Lusifa kabla ya ugonjwa wake wa dhambi kuweza kuenea? Lusifa alikuwa amepinga kwa kusema kwamba serikali ya Mungu ilikuwa haina haki. Alikuwa amesema uongo kumhusu Mungu. Kama Mungu angekuwa amemwangamiza Lusifa wakati ule ule, basi, malaika wale wangekuwa wameanza kumtumikia yeye [Mungu] kwa hofu badala ya kumtumikia kwa upendo. Hilo, kwanza kabisa lingekuwa limelivunjilia mbali kusudi la Mungu la kuwaumba viumbe wenye uwezo wa kuchagua.

Mtu ye yote angewezaje kujua kama njia ya Mungu ilikuwa kweli bora kuliko zote? Mungu alimpa Shetani nafasi ya kuonyesha mfumo wake mbadala. Hii ndiyo maana alipewa fursa [nafasi] ya kumjaribu Adamu na Hawa.

Sayari hii imegeuka na kuwa uwanja wa majaribio ambamo hulinganishwa tabia ya Shetani na aina ya ufalme wake na tabia ya Mungu na aina ya Serikali yake. Nani mwenye haki? Ni nani tuwezaye kumtegemea mwishowe? Lusifa alikuwa mdanganyifu mno, hata imechukua muda kwa viumbe wa malimwengu kuweza kusadiki kabisa jinsi ilivyo hasa ile njia mbadala iletayo maafa aliyoichagua Shetani. Lakini hatimaye kila mtu atatambua kwamba "mshahara wa dhambi ni mauti" na ya kwamba "karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu" (Warumi 6:23).

Kila kiumbe katika malimwengu hayo wakati ule kitakubali kwamba:-
"Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi. Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee mfalme wa mataifa.... mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa" - (Ufunuo 15:3,4).

Baada ya kila mtu kuielewa tabia ya kufisha ya dhambi na hali ya uharibifu inayoletwa na falsafa ya Shetani, ndipo Mungu anaweza kumwangamiza Shetani pamoja na dhambi. Atalazimika pia kuwaangamiza wale ambao kwa ukaidi wao wanapinga neema yake na kuing'ang'ania ile njia mbadala aliyoiweka Shetani.

Mungu anahangaika vile vile kulitatua tatizo hilo la dhambi na mateso kama sisi tunavyotaka yeye afanye hivyo. Lakini anangojea mpaka hapo atakapoweza kufanya hivyo kwa msingi utakaoleta matokeo ya kudumu, na mpaka hapo anapoweza kuuhifadhi uhuru wetu wa kuchagua na kuuzuia uovu usipate kutokea tena.

Mungu ameahidi kuiangamiza dhambi milele kwa njia ya kuzitakasa mbingu na dunia hii kwa moto. "kama ilivyo ahadi yake" tunaweza ku"tazamia mbingu mpya na nchi mpya, makao ya wenye haki" (2Petro 3:10,13). Dhambi haitaenea kamwe katika malimwengu kwa mara ya pili. Matokeo mabaya sana ya dhambi yataonekana wazi kabisa kiasi kwamba uasi dhidi ya Mungu utaonekana kuwa ni wa kuchukiza milele zote.

Je, ni nani anayefanya uwezekano uwepo wa kumwangamiza Shetani pamoja na dhambi?
"Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye [Kristo] vivyo hivyo alishiriki katika ubinadmu wao, ili kwa njia ya mauti apate kumharibu yeye aliye na nguvu za mauti - yaani Ibilisi - awaache huru wale ambao katika maisha yao yote walikuwa wameshikiliwa katika hali ya utumwa kwa hofu yao ya mauti" - (Waebrania 2:14,15).

Pale msalabani malaika pamoja na wale wa dunia zisizoanguka dhambini walimwona Shetani kama alivyo hasa - laghai, mwongo, mwuaji. Pale ndipo alipoidhihirisha tabia yake halisi kwa kuwalazimisha wanadamu kumwua Mwana wa Mungu asiye na hatia. Wakazi wa malimwengu yote walijionea wenyewe jinsi dhambi isivyo na maana kabisa na ilivyo katili kama vile ilivyo hasa. Msalaba uliyafichua kabisa makusudi ya Shetani, na Mungu atakapomwangamiza Shetani pamoja na wale wanaoendelea kutenda dhambi, wote watakiri kwamba Mungu ni mwenye haki.

Kifo cha Yesu pale msalabani kilifunua wazi mbele ya viumbe wote walioumbwa kusudi halisi alilonalo Shetani (Yohana 12:31,32). Pia msalaba ule ulimfunua Kristo alivyo hasa - yaani, yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Pale Golgotha nguvu ya upendo ilijitokeza wazi kabisa dhidi ya kupenda mamlaka. Msalaba ule ulithibitisha bila shaka lolote kwamba ni ule upendo unaojitoa kafara ambao unamsukuma Mungu katika kushughulika kwake kote na Shetani, dhambi, pamoja na wanaume na wanawake wenye dhambi.

Pale msalabani Kristo alionyesha upendo wa Mungu usio na masharti kwa njia iliyokuwa na uwezo wa kuushawishi moyo na kumshinda kabisa Shetani. Vita ilikuwa juu ya nani atakayeitawala dunia hii, Kristo au Shetani? Tena, msalaba ule uliamua hoja hiyo kwa wakati wote. Ni lazima awe Kristo juu ya wote!

Je, umeugundua uhusiano wako na Mwokozi aliyekufa ili kuudhihirisha upendo wake usio na kifani, ambao haubadiliki? Unajisikiaje kuhusiana na huyo mmoja aliyekuja katika dunia yetu kama mwanadamu, na kufa badala yako ili kukuokoa wewe mbali na matokeo ya dhambi? Je, utainamisha chini kichwa chako hivi sasa na kumshukuru Yesu, na halafu kumwomba aingie ndani na kuyatawala maisha yako?.....................


© 2004 The Voice of Prophecy Radio Broadcast
Los Angeles, California, U.S.A.